Nenda kwa yaliyomo

MDMA

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

MDMA (3,4-Methyl​enedioxy​methamphetamine, inayojulikana sana kama ecstasy (E) au molly) ni dawa inayoathiri akili ambayo hutumika kimsingi kwa madhumuni ya burudani. Athari yake ni pamoja na mihemko iliyobadilika, nguvu iliyoongezeka, huruma na raha. Inapochukuliwa kwa mdomo, athari zake huanza baada ya dakika 30 hadi 45 na hudumu kuanzia saa 3 hadi 6.

Madhara yake ni pamoja na uraibu, matatizo ya kumbukumbu, kutokuwa na imani na wengine bila uhalisia (paranoia), kukosa usingizi, kusaga meno, uoni hafifu, kutokwa na jasho na mapigo ya moyo ya haraka. Vifo vimeripotiwa kutokana na ongezeko la joto la mwili na upungufu wa maji mwilini. Kufuatia matumizi yake mara nyingi watu huhisi huzuni na uchovu. MDMA hufanya kazi hasa kwa kuongeza shughuli za chembe za nyurotransmita serotonini, dopamini na noradrenalini katika sehemu za ubongo. Dawa hii ni ya makundi ya amfetamini yaliyobadilishwa ya madawa ya kulevya na ina athari za kichocheo na kuleta njozi.

MDMA ni kinyume cha sheria katika nchi nyingi, na kufikia mwaka wa 2018, haina matumizi ya matibabu yaliyoidhinishwa. Vighairi vichache wakati mwingine hufanywa kwa ajili ya utafiti. Watafiti wanachunguza ikiwa MDMA inaweza kusaidia katika kutibu ugonjwa mkali, sugu wa mkazo wa baada ya kiwewe (PTSD) na majaribio ya kikliniki ya awamu ya 3 ili kuangalia ufanisi na usalama wake unaotarajiwa kuanza katika mwaka wa 2018. Mnamo mwaka wa 2017, FDA iliipa MDMA uteuzi wa tiba ya mafanikio kwa ajili ya PTSD, kumaanisha kwamba ikiwa tafiti zitakuwa nzuri, basi mapitio ya matumizi yake ya kimatibabu yanayoweza kutokea yanaweza kutokea kwa haraka zaidi.

MDMA ilianzishwa mwaka wa 1912 na Merck. Ilitumika kuimarisha tiba ya kisaikolojia kuanzia miaka ya 1970 na ikawa maarufu kama dawa ya mitaani katika miaka ya 1980. MDMA kwa kawaida huhusishwa na karamu za densi, vilabu, na muziki wa dansi wa kielektroniki. Inaweza kuchanganywa na vitu vingine kama vile efedrini (ephedrine), amfetamini, na methamfetamini (methamphetamine). Mnamo mwaka wa 2016, takriban watu milioni 21 kati ya umri wa miaka 15 na 64 walitumia dawa hii (0.3% ya idadi ya watu ulimwenguni) Hii ilikuwa sawa na asilimia ya watu wanaotumia kokeini au amfetamini, lakini chini kuliko waliotumia bangi au afyuni Nchini Marekani, kufikia mwaka wa 2017, karibu 7% ya watu walikuwa wametumia MDMA wakati fulani katika maisha yao, na 0.9% walikuwa wameitumia mwaka uliopita.