Madoa ya Jua
Madoa ya Jua ni sehemu kwenye uso wa Jua zinazoonekana nyeusi-nyeusi katika darubini ya mtazamaji. Madoa makubwa yanaweza kutazamiwa pia wakati wa machweo kwa macho matupu. Sehemu hizi huwa na jotoridi duni kulingana na maeneo mengine kwenye uso wa Jua na hivyo zinatoa kiwango kidogo zaidi cha nuru kinachosababisha kuonekana tofauti. Idadi ya madoa ya jua inabadilikabadilika kwa kufuata duru yaani mpangilio wa kurudia kila baada ya miaka 11.
Madoa yanasababishwa na mabadiliko ya ugasumaku katika tabakanuru ya Jua zinazoathiri miendo ya joto ndani yake. Penye doa la Jua ugasumaku unapindwa na kupita takabanuru ikielekea nje. Kawenye sehemu hizi uso wake ni mkubwa hivyo eneo hili linapoa kushinda mazingira ya jirani na tofauti hii inaonekana kama "doa".
Hali halisi ya madoa si „ nyeusi“ ila jotoridi hapa ni takriban nyuzi za Kelvini 1500 chini ya jotoridi ya kawaida kwa hiyo inatoa asilimia 30% tu ya kiwango cha kawaida cha nuru kwa kulingana na wastani wa uso wa Jua.
Katika vipindi venye madoa mengi pia ugasumaku ya Dunia inaathiriwa; hali hii inaonekana katika mwingiliano wa mapokezi ya redio na mawasiliano kutoka satelaiti.
Wataalamu bado wanajadili kama kuongezeka kwa madoa ya Jua kunaweza kuleta mabadiliko katika tabianchi duniani.